CHEKACHEKA

Mwandishi: T.A.Mvungi
Wachapishaji: EP & D.LTD

Maudhui

Tunaweza kujadili dhamira za Mashairi ya Cheka Cheka katika mfululizo ufuatao:

  • Siasa
  • Mapenzi
  • Dini
  • Mengineyo

(a) Siasa

Hii ni dhamira inayomgusa mwandishi kwa kiasi kikubwa. Mawazo ya kisiasa ya mshairi huyo yanajitokeza pia katika mashairi yake mengine kama vile Raha Kara, Chungu Tamu na kadhalika. Sauti ya mshairi huyo kila mara imejitokeza kwa ukali kabisa.

Kutetea Haki

Katika shairi la “Mwinyi Umewasha Moto” (uk.l), mshairi anamwomba Raisi Ali Hassani Mwinyi kuwa imara na kulinda 'moto' aliouwasha. Ni moto gani huo? Ni kujali haki na kufanya ukali wa kuleta haki hiyo.

Raisi Mwinyi anahimizwa kuwa mkali kwani nchi yetu ni ya mazonge. Tunamsikia akisema:

"Tumaini la wanyonge, kwamba ipo serikali
Ila nchi ya mazonge, ya wenye meno makali
Wanyang'anyao matonge, wanyonge hawana hali
Mwinyi ukiwa mkali, ndio raha ya raia"

Wakati wowote, kushindwa au kuondolewa madarakani ni kitu kibaya. Kwa kuzingatia jambo hilo, mshairi anatahadharisha kwa Raisi kuwa:

"Wale unaokusudia, kuwatoa kwenye viti
Kwa kweli wanachukia, sasa wanajizatiti!"

Ndiyo maana hata baadhi ya nchi mbalimbali hupinda Katiba ili kuwafurahisha watawala. Kwa hiyo Raisi awe mwangalifu. Watu hawa ni sawa na nyoka aliyechokozwa na ambaye lazima auawe.

Demokrasia

Mawazo juu ya demokrasia nchini yamejitokeza sehemu mbalimbali, lakini yanaelekea kupewa uzito mkubwa sana katika shairi la Taifa Wamelizika. Katika shairi hilo mshairi kwanza anatoa mwito kwa wajumbe walio katika chama cha CCM ambao huingia Bungeni, ama wale waendao mikutanoni wapunguze blabla nyingi katika hotuba zao. Kwa mara nyingine tena inadhihirika kuwa baadhi ya watu hawajui maana ya demokrasia. Demokrasia sio kupiga kelele zisizo na maana au zisizotekelezwa.

Hali ya kuwa bendera kufuata upepo mshairi anaikataa. Kuna wale wajumbe wenye maneno mazuri jukwaani, lakini utekelezaji wa maneno yao ni finyu. Wao wanajali utukufu wao, furaha zao, lakini hawaoni hangaiko la raia.

Mifano mingine inayotolewa ni ile inayohusu maduka yaliyokuwa hayana vitu na ambayo yalikuwa (enzi ya miaka 1979 - 1988) yakitegemewa na wananchi wa kawaida. Kuna maelezo kuwa kila pale raia walipokuwa wakihangaika, tabaka la juu - yaani tabaka tawala lilikuwa halijali.

Siasa ya Chama kimoja

Mshairi anaona kuwa tabia ya kuwa na Chama kimoja tu cha kisiasa inawanyima watu uhuru na demokrasia. Mshairi anaona:

  • " Mezikwa demokrasi, Chama kimoja ndo' ngao
    Watu hawana nafasi, kutetea nchi yao
    Mawazo ya ukakasi, mawazo ya mtitio "
  • Hivyo ndivyo anavyoona yeye. Juu ya hofu ya kuwa na vyama vingi, mshairi anasema:

    " Waogopao vingi vyama, ni hofu ya kuumbuka
    Maovu wanayofuma, kwa dharau na dhihaka
    Vyama vingi vingesema, na kutwaa madaraka
    Pasipo uhuru huo, utu upo mashakani"

    Mshairi (kabla ya kuruhusiwa mfumo wa vyama vingi) analalamika na kushtumu hali iliyopo chini ya kung'ang'ania kuwa na chama kimoja. Kwa mtazamo wake, wananchi wanakosa uhuru wa kuikosoa serikali yao kwa undani, kwani chama kimoja kinazuia uhuru huo. Viongozi hufanya hivyo ili kuukwepa ukweli wa mawazo ambayo yangeweza kutolewa kama kungekuwa na vyama vingi. Sasa vyama vingi vimeruhusiwa. Tunategemea matakwa ya mwandishi yatekelezwe.

    Aidha, parnoja na shutuma hizo, yaelekea mshairi kaona uzito wa hoja kuwa vyama vingi vinaweza kuleta matatizo ya kijamii nchini. Kuna mawazo ya baadhi ya wananchi kwa mfano yanayodai kuwa kama nchi yetu ikiruhusiwa kuwa na vyama viwili au vitabu vya kisiasa, mambo yafuatayo yanaweza kutokea; na ni vema yapigwe vita.

    • Mgawanyiko wa watu kwenye chama cha kisiasa ambacho kitakuwa na kina athari ya madhehebu ya dini ya aina fulani.

    • Mgawanyiko wa watu kwenye chama cha kisiasa ambacho kitakuwa na kina athari ya ukabila.

    • Mgawanyiko wa watu kwenye chama cha kisiasa ambacho kitaigawa nchi katika kanda mbili au zaidi.

    Tahadhari hizi zilizopata kutolewa na baadhi ya wanasiasa, hazielekei kukubalika kwa mashairi. Katika ngazi hii, yaelekea mshairi ameguswa na kuathiriwa na mihemko zaidi kuliko kuangalia mambo katika hali halisi. Pengine ni muhimu kutambua kwamba hakuna zuri lisilokuwa na ubaya wake! Kinachotakiwa ni kuangalia uwiano na uafadhali wa mawiano hayo katika uhalisia wa maisha. Vyama vilivyoanzishwa visiwe vya kisasi dhidi ya Chama cha CCM. Vyama hivi pia viwe “dhati” na siyo vyama vya kidini au kikabila vyenye vurugu.

    Rushwa na Ulanguzi

    Kama ilivyojitokeza katika diwani nyingine za mshairi huyo, tatizo la rushwa na ulanguzi linaelekea kujadiliwa tena kwa undani katika diwani hii. Imedhihirika wazi kuwa suala la rushwa na ulanguzi linaendeshwa na kusimamiwa na watu wakubwa kwenye serikali na mashirika ya umma. Katika kufanya uharamu wao, walanguzi wameweza kujinufaisha sana; wengine wana magari, wengine wana majumba makubwa makubwa, na wengine kila siku wana maisha ya anasa na kifahari. Wakati wote huu, wakulima na wavuja jasho ama 'walala hoi' wengine wanazidi kudidimia na kuteseka katika maisha yao. Dawa ya kukomesha haya na adha zote hizo, mwandishi anapendekeza kuwa ni:

    ....... walaji wapigwe vita,
    ....... hawa dawa yao radi,

    Mwinyi unda zako mbinu, iwe dawa ya kudumu (uk. 1)

    Ingawa mshairi anapendekeza dawa ya kukomesha haya yote ni radi, yaelekea hilo halikutekelezwa. Matokeo yake, mashirika na miradi mbalimblai imetindia na mingine kufa kabisa. Hivi sasa kuna wito karibu kila siku wa kufanya ubia na mashirika au kampuni za nje. Ni kwa kiwango gani hali hii itanutaisha taifa? Tunasubiri!.

    Matumizi ovyo ya Fedha za Umma

    Kashfa ya mtumizi mabaya ya fedha katika vyombo ama mashirika ya umma na serikali ni jambo la kawaida sasa hapa nchini. Katika kutumia ovyo fedha hizo, baadhi ya viongozi wanajipangia masurufu makubwa makubwa kila wakiwa mwenye mikutano. Baadhi ya mikutano hiyo kwa hakika siyo ya lazima sana, ni njia mojawapo ya kuangamiza fedha za umma tu!

    "Sherehe zenye utamu, raha za wachache
    Ni mateso ya kaumu, wasoweza kujikimu
    Mikoa yafanya zamu, kuziandaa karamu"
    (uk. 27)

    Wananchi ndio wanaoandaa sherehe. Lakini wanaofaidi furaha hizo hasa ni watu wachache - na hivyo kuacha wananchi waendelee kuteseka.

    Uzembe na Ukasuku

    Katika shairi la Ni wa Wapo Mshairi anaelekea, pamoja na mengi mengineyo kukemea uzembe. Uzembe umesababisha mazao ya wakulima kulundikana ovyo bila kusafirishwa na kuuzwa Jije!. Mazao kama vilepamba, mahindi, ufuta ni mifano michache iliyotajwa.

    Kama kila mtu angekuwa anawajihika bila kusukumwa baada ya kuzembea hali isingekuwa hivyo.

    Mshairi anawaona baadhi ya watu wana tabia ya ukasuku. Wakipata jambo hupenda kuliimba bila hata kulichambua na kulifanyia utafiti wa kufaa.

    Katika kusisitiza hoja yake, mshairi anawahimiza wasanii kuwa kama nyati. Tunaisikia sauti ya mshairi ikidai katika Tuambae Ukasuku hivi:

    "Kadhalika tafakari, Mshairi uwe nyati
    Laghai usiwakiri, wasikura kwa nyati
    Ati ukweli ni shari, uwapigie magoti
    Kataa hotuba tupu, Kandamiza la jamii"
    (uk. 3)

    Hoja ya Jumla

    Mshairi amejitahidi sana kuichambua jamii ya Tanzania (ingawa yaliyosemwa yanaweza kuwahusu wengine nje ya Tanzania) na kutoa hali halisi. Swali ni je? Ni wangapi nchini wanakifahamu kilio cha mwandishi? Wana uamuzi gani? Kilio chamwandishi juu ya hali mbaya ya nchi kinasikika mahali pengi kwenye diwani hii: “Raia si Malikitu” (Uk. 5) “Mwinyi” (uk. 1), “Taifa” (uk. 2), na kadhalika.

    Mapenzi

    Kama ilivyo katika diwani zake nyingine, dhamira hii inajitokeza tena katika diwani hii.

    Mashairi yaliyojitokeza wazi kubeba dhamira hii ni pamoja na “Njiwa Kiumbe Mtini” (uk. 12) “Kimoyo” “Penzi lisilo Heshima” (uk. 15).

    Katika shairi lake la Njiwa Kiumbe Mtini tunamwona mshairi akitoa hisia zake kali kuhusu 'Njiwa' aliye mtini. Kimsingi, mshairi hapa ametumia tamathali maalumu ya kitashihisi na kusababisha kujenga taswira kwa msomaji wake.

    Kwa nje tunaisikia sauti ya mshairi ikilalamika juu ya hamu ya kumtia 'Njiwa' mkononi na kuwa wake.

    "Yeye juu hurukia, namuomba samahani
    Nyimbo ananiimbia, nyimbo zachoma moyoni
    Basi mie taabani, njiwa akitabasamu."
    (uk. 12)

    Katika lugha ya kawaida, tungeweza kusema kuwa mshairi anamlalamikia mpenzi wake ambaye anamtesa kila akijaribu kumchukua.

    Mshairi katika kuelezea mapenzi yake kwa kumtumia 'Njiwa' tunamwona akijitahidi kujenga taswira ya njiwa anayeruka hapa na pale matawini kwa lengo la 'kumjaribu' mshairi kama anavyosema mwenyewe:

    " Si kwamba anikimbia, ni mbinu zake teule
    Tabu kuniongezea, hata chakula nisile.
    Njiwa kushuka hashuki, na mtini haondoki,"
    (uk. 12)

    Hali hii inafanya mshairi asononeke. Tunaweza kumwona 'njiwa' wa mshairi aliyeng'ang'ania mtini asiondoke na uzuri wake. Tunaweza pia kumwona mshairi akisononeka pale chini ya mti huku akiwa na tamaa kubwa ya kumpata 'njiwa' aliye mtini.

    Tungeweza kusema katika lugha ya kawaida kuwa mshairi ana mpenzi wake ambaye anampenda, lakini kila akitaka kukamilisha mipango ya kuishi pamoja; uamuzi wa huyo mpenzi huwa wataratibu!.

    Mwishowe, mshairi anamwomba 'Njiwa' asimtese zaidi:

    Unayofanya si kweli, njiwa wacha tafrani
    Moyo waunyima hali, kwanini unauhini
    Rudi usiende mbali, moyo uwe ufueni
    Njiwa hebu baini, moyo unavyoteseka (uk. 12)

    Mapenzi yasiyo yakweli

    Mshairi, katika shairi lake la 'Penzi lisilo Heshima' (uk. 15) anaingia ndani zaidi ya suala hili la mapenzi na kuelezea maana na kiwango chake. Penzi la kweli kwa maoni ya mshairi ni lile lisiloathiriwa na mambo kama vile fedha, nguo, gari na kadhalika. Lakini hali ikoje katika uhalisia? Ndipo anaposema:

    "Penzi la umasikini, kwa hii Dunia
    Ni penzi la nuksani, mpendwa hatapokea
    Mpendwa hamuelewani, kwa maneno kumwambia
    Mfukoni kuna kitu, mpenda wahangaika"
    (uk. 15)

    Ndoa nyingi kwa sasa zinayumba kwa sababu ya kuthamini pesa, ukwasi! Urafiki wa kawaida nao hivi hivi. Kwa maoni ya mshairi penzi lililokosa heshima ni lipi?

    "Penzi lisilo heshima, penzi ladai mapesa
    Sio mapenzi ni chuki, sio raha ni simanzi
    Mapenzi ya uzandiki, chanzo cha huu utunzi"

    Mapenzi ya kweli ndio yanayotakiwa. Watu waambizana ukweli, kwani Kweli ina mvutio, sio wongo wa kuvutana. Ni kauli ya kituo, kauli ya kupatana.

    (c) Dini

    Mara nyingi wasanii wanapozungumzia suala la dini wanakuwa waangalifu kwa kuzingatia kuwa jambo hili ni nyeti miongoni mwa wanajamii. Msanii amechukua tahadhari ya kutosha anapoligusa jambo hili.

    Jambo la dini linajitokeza katika shairi la Chanzo cha huo uozo (uk. 25). Katika shairi hili, mshairi anadai ameona uozo katika dini.mshairi anasema:

    " Nimeona upotofu, humu ukristoni
    Upotofu wenye hofu, wahubiri mu kundini
    Mlei na Askofu, nyote mfanye makini
    Dini iwe maadili, msisitizo si fedha."
    (uk. 25)

    Kwa kawaida, kila Jumapili kuna kipindi katika maombi ya misa ambapo waumini hutoa mchango wa fedha ili ziweze kutumika kwa shughuli za kanisa. Hakuna anayelazimishwa kufanya hivyo. Kuliweka suala hivyo lilivyowekwa ni kupotosha ukweli wa yale yanayofanyika katika dini hiyo.

    Hata hivyo, inawezekana kuna baadhi ya watu katika taasisi hiyo, kama vile mapadri waliotajwa na msanii wanakiuka misingi dini na kutia mkazo kwenye fedha. mshairi anasema:

    " Ninalaani mkazo, huu mkazo wa mali
    Mkazo una mzozo, unikumbushao mbali
    Chanzo cha huo uozo, husahau maadili
    Padili punguza hamu, ya shilingi kuzipenda"
    (uk. 25)

    Kwa upande mwingine ni vema ifahamike kuwa suala la dini ni suala la imani ya mtu. Kila mtu ni sabihi katika imani yake. Katika imani hiyo ni vema pia kujua kuwa kuna ubinadamu. Hakuna binadamu aliye kamili. Lakini pia, katika upungufu wa ukamilifu huo, binadamu anatakiwa aishi katika misingi na mazingira yanayokubalika. Mkristu azingatie misingi yake, na Muislamu naye azingatie misingi yake ya Uislamu. Hakuna mwenye haki nje ya mazingira yanayokubalika.

    Uhusiano wa Kimataifa

    Katika dhamira hii tunaweza kutoa mfano wa mashairi mawili, shairi la “Indira” (uk. 18) na “Utumwa Huru” (uk. 23).

    Katika shairi la Indira mwandishi anatoa hisia zake za kilio kwa kiongozi huyu shupavu aliyeuawa miaka michache iliyopita. Kitendo cha nchi au mtu kuonyesha hali kama hii iliyoonyeshwa na mshairi katika shairi lake kunaonyesha uhusiano muhimu. Tunamsikia mshairi akilia:

    "Wengi tumesononeka
    Oktoba kututoka
    Umeondoka haraka
    Kwa kweli ulitukuka "
    (uk. 18)

    Kitu muhimu ambacho kimemfanya mshairi, na labda jumuia ya mshairi kumsononekea 'shujaa' Indira Gandhi ni kuwa:

    "Haki ulipigania
    Pia demokrasia
    Vyama ulizingatia
    Ndio msingi imara"
    (uk. 18)

    Mawazo ya kutetea haki yanajitokeza pia katika shairi lake la Utumwa Huru (uk. 23)

    Katika shairi hili, mwandishi anaonelea - na kulaani dhuluma chafu za makaburu, zikiwemo ubaguzi wa rangi, ukandamizaji na kadhalika. Mshairi anaelezea adha za Kaburu kwa mfano:

    "Kaburu atenga rangi, ninyama yule katili
    Tena ana kwa wingi, katili hana akili
    Weupe ndio makingi, Mwafirika hatawali
    Ni uovu wa Kaburu, aibu barani kwetu."
    (uk. 13)

    Uhusiano huu mchafu miongoni mwa weupe na weusi wa Afrika Kusini utaleta madhara, hapawezi kuwa na utulivu hata kidogo!.

    Lakini mshairi bado anaelezea hisia muhimu zinazojitokeza katika mataifa mengine ya Kiafrika. Mshairi anasema kuwa hali ya ukandamizaji siyo ya Makaburu tu. Kuna weusi pia huwakandamiza ama kuwaua ovyoovyo weusi wenzao. Hali hii inampa kiburi Kaburu, anasikika akikebehi:

    "Ona tawala nyeusi, mbinu zao za utesi
    Ni neno demokrasi, lasisitizwa kwa kadi
    Sambamba nazo risasi, ni hotuba na utezi"
    (uk. 23)

    Halafu anaeleza wapi hasa dhuluma hizo zinashamiri sana:

    "Pale za Jeshi tawala, na pale chama kimoja
    Kule dini yatawala, kwa raia ni mamoja
    Ananyang'anywa chakula, na kuzimwa zake hoja
    Afrika vichekesho, kwa uhuru wa viroja"
    (uk. 23)

    Tahadhari yetu juu ya ubeti huu ni kwamba si lazima kila pale linapotawala jeshi au pale penye chama kimoja kuna dhuluma!

    Maisha

    Yako mashairi yanayoweza kuonekana na mawazo ya jumla kuhusu maisha ya mtu kwa ujumla. Mfano tunaoweza kuutoa hapa ni ule wa shairi la Utu Umekuwa Kima (uk. 19) na Dhahabu ya Fahari. (uk. 19).

    Katika shairi hilo, mshairi anaonya juu ya wale wanaodharau utu. Pia, anatahadharisha kuwa si kila ing'aayo ni dhahabu, na kwamba watu wanaweza kulikubaliajambo baya kwa lengo la kuiionyeshatu kwajamii kumbe wanakufa 'kiofisa'.

    Katika shairi lake la Utaliwa kama Pumba (uk. 21) tunamsikia mshairi akizungumzia mauti. Anaonekana kutishika nayo, na katika tisho hilo tunamsikia akisema:

    "Mauti nipishe mbali, ujitaye umoja
    Mauti uso akili, kila uchao viroja
    Mauti mwana katili, wewe usojali hoja
    Mimi nawe shirikani, mwiko! Haiwezekani."
    (uk. 21)

    Shairi hili kwa upande mwingine tunaweza kulisema ni la kitaswira. Mauti inayosemwa hapa yawezekana kuwa kitu kingine, lakini tabia ya 'Mauti' ubaya na hatari, tisho na unyanyaswi ni vitu anavyovikemea mshairi.

    Fani

    Muundo na Mitindo

    Vina

    Kuna aina mbili za vina: vya kati na vya mwisho. Baadhi ya mashairi, kama vile 'Indira' (uk. 18) yana vina vya mwisho tu. Aidha kuna vina vinavyotiririka kutoka ubeti wa kwanza hadi mwisho.

    Mizani

    Kama ilivyo kwenye vina, hapa kuna mashain ya mizani kumi na sita (16) katika mgawo wa 8/8. Aidha, yako pia mashairi yenye mizani minane (8) kila mstari (Utu umekuwa kina, uk. 19).

    Ubeti

    Kila ubeti katika mashairi hayo una mistari minne (4). Kuna pia mistari ya vituo.

    Msisitizo

    Kuna shairi moja ambalo limechukua mtindo wa msisitizo. Shairi hilo ni la 'Mtoto Aso Riziki' (uk. 27). Tukiondoa shairi hili, mashairi mengine yote ni ya kitarbia.

    Mazingira

    Mashairi yametumia mazingira ya kitanzania kwa mapana. Aidha, kuna mashairi kadhaa (Indira/Utumwa Huru) yamevuka mpaka wa mazingira ya Kitanzania.

    Wahusika

    Mashairi yanatumia wahusika watu. Aidha pale anapotumia wahusika 'vitu' au 'viumbe' kwa ujumla vitu hivyo ni viwakilishi vya tabia ya mtu.

    Matumizi ya Lugha

    Mshairi, kama ilivyo katika diwani zake nyingine anajitahidi kutumia lugha ya kishairi. Aidha, hajafanikiwa sana katika kipengele cha lugha. Tutajadili zaidi vipengele hivyo.

    Mbinu za Kisanaa

    Mkato wa maneno

    Mshairi anaonekana kukata maneno katika baadhi ya mashairi. Jambo hili aghalabu hufanywa na mshairi kwa madhumuni ya kulinganisha mizani katika shairi analolitunga. Katika hatua isiyo ya kawaida, mshairi anaweza kuongeza herufi moja au mbili katika neno la shairi ili kuunda vina vya aina ile anayoipenda mshairi. Aidha, hatua zote mbili zinaweza kuathiri katika hali zifuatazo.

    • Neno linaloundwa linaweza kupotosha maana
    • Neno linaloundwa linaweza kuonekana kimauinbile kuwa ni jipya.

    Mfano wa mkato wa maneno ni huu ufuatao kutoka shairi la Utumwa Huru (uk. 23).

    A 'lakini angalia, nyingine za Afrika,
    Lo, zana kuzidia, tawala zajisimika

    Tashtiti

    Mshairi ametumia mbinu hizo pia. Mfano unaweza kupatikana katika mashairi mbalimbali, likiwemo lile la 'Mtoto Aso Riziki' (uk. 27).

    Maneno yaliyotoholewa na yale ya Kikabila

    Yako maneno ambayo ni ya asili ya lugha nyingine, kama vile Kiingereza. Mfano unapatikana katika shairi la 'Chunguzeni walo Mbele' (uk. 17).

    Yako pia maneno yaliyochukuliwa kutoka katika makabila ya Kibantu.

    Takriri

    Mwandishi ametumia mbinu hii ya kurudiarudia maneno au miundo na kadhalika. Mbinu bii ambayo lengo lake ni kusisitizajambo linajitokeza pahala pengi. Tunaweza kuzikuta aina za takriri zifuatazo:

    • Takriri - Neno

      Tazama shairi la 'Moyo' (uk. 13). Neno moyo limerudiwa mara kadhaa.

      Moyo nimeushauri, lakini umekaidi
      Moyo kiburi hatari, mfanowe kama radi

      ....Moyo mefumbata sheria, unayokwepa marudi

      .....Mayo u mwilini mwangu, jirudi tuwe pamoja

    • Takriri Vina

      Kuna takriri vina -ri- na -di- katika ubeti huo
      Takriri nyingine ni mizani, silabi, mistari na miundo na kadhalika.

    Tamathali za Usemi na Ujenzi wa Taswira

    Mshairi ametumia tamathali za semi mbalimbali. Tamathali hizo zinasababisha kujengwa kwa taswira mbalimbali.

    Tashibiha

    Tamathali ya aina hii imetumiwa mara kadhaa katika mashairi mbalimbali. Mifano ya tashibiha ni hii iftiatayo:

    Na wasiothaminiwa, wapimwao kama nyasi (uk. 5)
    Mlevi akakolea, kaina lumbaku ya toza (uk. 7)
    Moyo kiburi hatari mfanowe kama radi (uk. 13)

    Tashihisi

    Tamathali ya aina hii ambayo hukifanya kitu kitende kama binadamu imetumiwa pia. Angalia mifano:

    Wewe kimoyo sikia, mbona unanipa tabu (uk. 12)
    Moyo jifunze busara, iwe ndiyo yako taa
    Moyo usiwe jeuri, makinika kwa hekima (uk. 13)
    Unayofanya si kweli, njiwa wacha tafrani

    Katika mifano hii michache tunaweza kuona mfano dhahiri juu ya tamathali hizo. Mfano wa awali kimoyo anaombwa asikilize, asimpe tabu (mshairi). Mfano wa pili, moyo anaambiwa ajifunze busara; na kuendelea. Aidha mfano wa mwisho tunaambiwa hadithi ya njiwa (ambaye kwa kweli ni mpenzi) aliye mtini na kumtesa (mshairi).

    Sitiari

    Hii ni tamathali inayolinganisha vitu vyenye sifa tofauti, lakini haitumii viungo kama ilivyo katika tashibiha. Mfano wa wazi ni huu ufuatao:

    Dhuluma ndiyo hekima
    Utu umekuwa kima
    Hafai huyo manyama
    Jumlaye ni uhuru

    Mfano mwingine ni huu unaofuata.

    Kadhalika tafakari, mshairi uwe nyati
    Nchi 'takumbwa najuto, la watu kuwa farasi

    Tamathali Nyingine

    Kuna pia tamathali ambazo zinajitokeza na kujenga taswira za kishairi.

    Ujewi wa Taswira

    Kama tulivyokwisha dokeza hapo awali, matumizi ya ishara, semi na tamathali za usemi yanasaidia sana katika ujenzi wa taswira. Diwani ya Mashairi ya Cheka Cheka ina taswira zinazojitokeza, japo si nyingi kama ilivyo katika diwani nyingine za washairi.

    Taswira za diwani hii zinaweza kuwa katika makundi mbalimbali: zionekanazo, za hisi, na za mawazoni.

    • Taswira Zionekanazo:

      Kwa upande huu wa taswira, tuna mifano michache. Angalia shairi la Tuambae Ukasuku (uk. 3) lilivyojenga taswira zake. Tutatumia beti zifuatazo.

      Hakuna athubutuye, ati nyati kumtuma
      Aibebe niizigoye, au chuchu kumkama
      Na sogi amjaziye, ampandishe kilima
      Nyati si mkubalifu, mfugaji atazikwa.

      Kadhalika tafakari, mshairi uwe nyati
      Ati ukweli ni shari, uwapigie magoti
      Mshairi jihadhari, usishikwe kama funbo
      Usiwe kama kunguru, woga umejaa tumbo
      (uk. 3)

    Katika mistari hiyo iliyodondolewa, tunaweza kuziona taswira muhimu za kimaumbile zinazojitokeza. Kwanza, tunaiona taswira ama picha ya nyati mkali ambayo 'mtu' hathubutu kumtuma mtu. Kuwa na ukali kama wa nyati si jambo la mchezo, ni la hatari. Tunaweza kuuona ukali wa nyati anayekamuliwa chuchu. Ni jambo la hatari.

    Katika hatua nyingine tunaisikia sauti ya mshairi ikisema: Usiwe kama kunguru. Kunguru ni ndege mwoga kwa kawaida. Kwa sababu ya woga wake anaweza kuruka hata akimwona mtu anainama tu - mtu ambaye hana kusudio lolote la kumdhuru.

    Halafu tunaambiwa pia mshairi asishikwe kama fimbo. Fimbo ikisha kamatwa haina uhuru. Na mshairi kushikwa kama fimbo ni jambo la kitumwa kabisa.

    • Taswira za Hisi:

      Taswira za aina hii si nyingi katika diwani hii, lakini ni muhimu kuzitaja pia. Katika shairi lake la 'Kuna Nini Huko Ndani' (uk. 4) tunaisikia sauti ya mshairi ikisema na kugundua harufu za kunukia. Kunukia huku kunaleta athari za hisia kali zinazosababisha mtu kuwa na tamaa kali zaidi. Mshairi anasema:

      Kuna nini huko ndani, mbona jiko lanukia?
      Rihi yajaa puani, na muda wajiendea
      Kisoiva kitu gani, mbona mate mwatutoa.
      Naona mwajigawia, mwapishi ninawahofu
      (uk. 4)

    Ubeti huu unaonyesha harufu inavyoathiri kwa kuibua hisia.

    • Taswira za Mawazoni:

      Taswira nyingine ni za mawazoni tu. Kwa mfanu, mshairi anatuletea shairi lake moja ambalo anaongea na 'kimoyo' (uk. 12) chake. Anasema kwa mfano:

      Wewe kimoyo sikia, mbona unanipa tabu?
      Si mimi wanionea, kwamba wewe yakusibu
      Ni pole nakuainbia, pole sina matibabu
      Kimoyo, sinilaumu, uwezo umekuwa haba
      (uk. 12)

    Ingawa tunajua kuwa kila mtu ana moyo, lakini mtu kuzungumza na moyo ni jambo la mawazoni tu. Linaathiri maisha ya mtu kwa kuzingatia kweli kwamba mtu huyo ana mgogoro na nafasi yake!

    1 comment: